Vyoo vya kutegemewa katika moja ya shule za sekondari hapa Tanzania |
Uwajibikaji ni moja ya dalili kuu ya
Uzalendo. Mtu aliye na sifa ya uzalendo, lazima awe muwajibikaji. Sekta nyingi
hapa Tanzania zinashindwa kupiga maendeleo yenye tija kwa sababu mbalimbali,
mojawapo na iliyo kuu ni kukosekana kwa uwajibikaji. Lengo la makala hii, ni
kujadili viashiria kadhaa vya kukosekana kwa uwajibikaji na uwajibishwaji katika
sekta ya elimu nchini Tanzania.
Wadau wote wa elimu kuanzia serikali na
mamlaka zake husika, wakuu wa shule, walimu, wazazi/walezi, jamii na wanafunzi
wenyewe wnahusika katika suala la uwajibikaji. Kila kundi lina nafasi yake na
wajibu wake katika kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Muhusika wa kwanza anayepaswa
kuwajibika ni mwanafunzi mwenyewe. Kuna ule msemo usemao, “unaweza kumlazimisha
punda kwenda mtoni, lakini siyo kunywa maji”. Shule inaweza kuwa na mazingira
rafiki ya kusomea, walimu wa kutosha na walio na vigezo, wawajibikaji na
uongozi bora, na uwepo wa nyenzo muhimu za kusomea na kujifunzia, lakini kama mwanafunzi hayupo tayari, ni bure
kabisa. Mwanafunzi anapaswa kujitambua, kujua anahitaji nini na kwa namna gani
atapata kile anachokihitaji. Katika
utafiti wake uliolenga kuangalia uhusiano
uliopo kati ya kujitambua kwa mwanafunzi
na mchango wa wazazi unavyoweza kuathiri ufaulu wake, Bhat (2013) amegundua kuwa, mwanafunzi anapojitambua/ jielewa
humpelekea kuwa na matokeo mazuri darasani.
Mtafiti huyu anatukumbusha kuwa,
kuwasaidia wanafunzi kujitambua ni jukumu nyeti sana la serikali, wakuu wa
shule, walimu, wazazi/walezi, na jamii
kwa ujumla. Uwekezaji wa kina wa kuhakikisha wanafunzi wanajitambua mapema
kunaweza kuwa ni moja ya muarobaini wa kuondoa tatizo la matokeo mabaya ya
mitihani mashuleni.
Bila kuwa na uwezo wa kujitambua, ni
vigumu kupata wanafunzi watakaoweza kuelewa kuwa kuna upungufu wa vitabu katika
shule yao, na hivyo kulazimika kutumia nguvu ya ziada, ikiwemo ya kuwa na moyo
wa kusafiri umbali mrefu hadi shule nyingine ili kupata vitabu alivyovihitaji,
au kufanya majaribio kadhaa ya maabara yaliyoshindikana shuleni kwake. Tatizo haliishii
tu kwenye upungufu wa maabara au kukosekana kwa maktaba iliyojitosheleza (ni
wanafunzi wangapi wanatumia maktaba za mikoa?), kwani hata masomo yasiyohitaji
maabara, matokeo si ya kuridhisha. Mwanafunzi mwenyewe ni moja ya tatizo.
Wanafunzi wengi wa shule za msingi na sekondari
wanahitaji mwongozo katika kujitambua. Kwa bahati mbaya sana, katika shule
zetu, hakuna watu na ofisi maalum za ushauri nasaha. Mara nyingi, kitengo hiki
muhumu hupewa mwalimu aonekanaye ana nidhamu nzuri ya kazi na busara. Hili ni
tatizo kubwa, kitengo hiki kina watu mahususi ambao kwao ni kazi yao na
wamebobea. Serikali haina budi kuwekeza katika hili. Hili likiwezekana, utakuwa
ni mwanzo wa kupata jamii ya watu wanaojitambua, wawajibikaji (wanaokubali
kuwajibishwa) na wazalendo.
Wazazi nao wana wajibu mkubwa sana
katika kuhakikisha watoto wao wanafanikiwa katika masomo yao. Zipo namna nyingi
ambazo mzazi anapaswa kuwajibika. Baadhi nimeshazigusia katika makala hii hapa.
Hapa nitagusia wajibu uliopo kati ya mzazi na shule asomayo mwanae. Wazazi
wanaonesha kutotimiza wajibu wao kwa kushindwa kuhoji shule husika kulikoni
matokeo ya wanafunzi wao kuwa mabaya tofauti na matarajio yao. Kukosekana kwa
uwajibikaji huu sio tu kwa wazazi lakini pia hata kwa mamlaka husika
zinazosimamia elimu, wakuu wa shule na walimu husika wa masomo.
Kunapokuwa na matokeo mabovu, kila
mmoja humtupia lawama aliye juu yake. Siyo mwalimu wa somo, siyo mzazi, siyo
serikali, kila mmoja ananawa mikono. Hakuna anayetaka kujitazama wala
kujiwajibisha, na hakuna wa kumuwajibisha mwingine. Siku za hivi karibuni,
shule za serikali zimekuwa na matokeo mabaya. Wanafunzi wanamaliza elimu ya
msingi bila kujua kusoma wala kuandika. Wazazi wanalipokea jambo hili bila
kuhoji. Hawatimizi wajibu wao wa msingi. Walimu nao wanaona ni kawaida, mzazi
aliyezaa atajua mwenyewe, nani kamwambia azae mtoto asiyeelewa. Hafikiri kuwa anaweza kuwa sehemu ya tatizo.
Katika hali ya kushangaza, pamoja na
ongezeko la shule nyingi za watu binafsi, ambazo zlilitegemewa kutoa huduma
nzuri, baadhi ya shule hizi zimekuwa na matokeo mabovu. Utozaji wa ada kubwa ni moja ya utambulisho wa
shule hizi. Si wazazi, wala serikali inayoziwajibisha baadhi ya shule hizi
zilizo na matokeo mabovu na miundo mbinu isiyofanana na matarajio ya wengi. Zipo
shule binafsi zisizo na uongozi makini, walimu wenye vigezo, zisizo na maabara
nzuri, maktaba na zisizowajali wafanyakazi wake lakini hakuna anayeziwajibisha
wala yeyote kuwajibika.
Bila shaka wazazi huwapeleka watoto wao
kwenye shule hizi bila kuzifahamu vyema huku wakiaminia uwezo wa vijana wao bila
kujua kuwa, mazingira yanaweza kuathiri masomo yao. Kwa kutokujali, wazazi
hupokea matokeo mabovu ya watoto wao na kutafuta namna nyingine ya
kuwaendeleza, ikiwa ni pamoja na kumuwajibisha mototo. Mzazi anashindwa
kufahamu pia, anapaswa kuihoji shule kufuatia matokeo mabovu ya mototo. Hii
huweza kumsaidia mzazi kuchukua hatua sahihi dhidi ya mtoto wake.
Katika mtandao mmoja wa kijamii, nimekutana
na madai ya walimu wanaodai kunyanyaswa na mwajiri wao kwa mkataba wao kuvunjwa
bila kufuata taratibu. Mwajiri amekosa kuwajibika, nani amwajibishe? Wahusika wa
kumuwajibisha wanalifahamu hili (kupitia mtandao wa kijamii?) kama kweli lipo?.
Walimu nao wanawajibika lakini kwa njia ambayo siyo ya moja kwa moja. Kwa nini
wasiende kwenye mamlaka husika? Pengine wameshaenda au wanajua namna wasivyo
wawajibikaji, na hivyo wamehitaji nguvu ya wananchi na mwingine yeyote
anayehusika ama kuguswa!
Moja ya idara muhimu za kujua
mustakabali wa walimu na mazingira wanayofanyia kazi ni idara ya Ukaguzi wa
shule. Wakaguzi wa shule ni kiungo muhimu kati ya shule, walimu na serikali.
Idara ya ukaguzi ni moja ya idara muhimu sana katika kuhakikisha elimu bora
inatolewa mashuleni, ikiwa ni pamoja na kulinda maslahi ya walimu. Shule binafsi
zinapaswa kufikiwa na wakaguzi na wafanye kazi yao kizalendo. Watoe taarifa
sahihi kwa kuzingatia uhalisia wa shule.
Serikali itemize wajibu wake wa kuziwajibisha shule za binafsi zinazowatoza
wazazi ada kubwa bila kujali ubora wa elimu wanayotoa.
Mazingira ya kutokuwajibika ni mengi, kama haya ya shule ya Marasibora
ya ukosefu wa vyoo, madawati na nyumba za walimu, yaliyoripotiwa na gazeti la
Tanzania daima mapema mwaka huu mwezi wa nne. Inaonekana hakuna anayetaka
kukubali kuwa hakuwajibika na hakuna akubaliye kuwajibishwa. Wakati mwingine, watumishi hupata kiburi cha kutowajibika kwa kuwa, mamlaka ya juu haijawajibika, yaani wanakomoa. Imefikia mahali sasa ule msemo wa “usiulize nchi yako itakufanyia nini, bali ujiulize wewe utaifanyia nini nchi yako”, umegeuzwa na kuwa, “wakati ninafikiri niifanyie nini nchi yangu, nayo nchi yangu haina budi kufikiri kama inanijengea mazingira sahihi ya kufikiri nitaifanyia nini”. Yawezekana msemo huu una mantiki. Akuandaliaye shibe usimkombee mboga. Hata mzazi, shibe ya njaa yake ni kuona kuwa watoto wake wameshiba. Tuwajibike, tukubali kuwajibishwa tunaposhindwa kujiwajibisha. .