Vifo Vya Akina Mama Kutokana Na Matatizo Ya Ujauzito(Maternal Mortality) ni tatzo kubwa Tanzania : Nini kifanyike kutatua tatizo hili?


Mbali na jitihada za dhati zinazofanywa na serikali yetu kwa muda mrefu kutatua tatizo la vifo vya akina mama kutokana na matatizo ya ujauzito (martenal mortality), takwimu za karibuni zinaonyesha hali sio nzuri kwani vifo vya akina mama vinaendelea kuongezeka kila mwaka. Bila ya mikakati thabiti kuelekezwa katika kutatua vyanzo vya tatizo hili kuna uwezekano wa kuendelea kuwapoteza; mama zetu, dada zetu, shangazi zetu na hata mabinti zetu kila siku. Hakika kila mtu anaguswa na vifo hivi, hivyo basi hatuna budi kushiriki katika kupeana mawazo ya jinsi ya kutatua tatizo hili.

Je vifo vya akina mama kutokana na matatizo ya ujauzito ni tatizo nchini? Ndiyo! Ni tatizo, tena ni tatizo kubwa sana, na hasa ukizingatia kwamba tatizo hili limekuwa sugu kwa muda mrefu hapa nchini Tanzania. Bado miaka mitano tu kufikia mwaka 2015, mwaka ambao malengo ya maendeleo ya millennia (MDGs) yamepangwa kufikiwa,Kuna matumaini madogo sana kwamba serikali ya Tanzania itaweza kufikia lengo la 5 (MDG 5) – kupunguza vifo vya akina mama kutokana na matatizo ya ujauzito kwa asilimia sabini na tano kati ya mwaka 1990 na 2015.

Takwimu za sensa ya afya za mwaka 2004 (TDHS 2004) zinaonyesha vifo vya akina mama kutokana na matatizo ya ujauzito vimezidi kuongezeka nchini Tanzania, kutoka vifo 529 kati ya akina mama 100,000 wanaojifungua katika mwaka 1996 mpaka kufikia vifo vya akina mama 578 kati ya akina mama 100,000 wanaojifungua katika mwaka 2004. Hivyo inaonyesha basi pamoja na jitihada zote za serikali kuondoa tatizo hili bado linaendelea kuongezeka siku hadi siku na hivyo tunazidi kupoteza maisha ya wapendwa wetu!. Na zaidi ya hili ni muhimu kujua kwamba zaidi ya akina mama 250,000 wanapata vilema vya kudumu kila mwaka kutokana na matatizo ya uzazi .Idadi hii ni kubwa, inatisha na inahitaji dhamira ya dhati kuondokana na tatizo hili.

Kuna jitihada zozote za kutatua sababu za vifo hivi? Ndiyo!Baadhi ya jitihada zinazofanywa na serikali ni kama kuongeza vyuo vya udaktari, wauguzi n.k ili kutatua tatizo la upungufu wa watoa huduma, Serikali imejitahidi pia kupeleka madawa na vifaa vya tiba kufikia ngazi ya zahanati ili kupunguza uhaba huo, pia imepitisha sheria ya kuruhusu huduma za ujauzito na huduma za rufaa (gari la wagonjwa) kutolewa bure ili wajawazito wengi wapate huduma salama, na inaendelea na mchakato wa kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa jamii kupitia wizara yake ya afya.

Maeneo ambayo bado yanaleta utata na kuhitaji ufumbuzi wa haraka?
1. Mbali ya jitihada zote zinazofanywa na serikali, watu binafsi na vyama vya kiraia vifo vinaendelea kuongezeka, nini hasa ni sababu ya tatizo hili? nini cha zaidi kifanyike?
2. Ni muhimu kujua kwamba ni asilimia 46% tu ya akina mama Tanzania wanajifungulia kwenye vituo vya afya? Tutaibadilisha vipi hali hii?
3. Mbali na sheria ya huduma za kujifungua ( pamoja na huduma za rufaa) kutakiwa kutolewa bure katika vituo ya afya vya serikali, bado hali inaendelea kuwa mbaya , tatizo ni nini? nini kifanyike zaidi?
4. Iko wapi nafasi, na kikomo cha wakunga wa jadi katika mfumo mzima wa utoaji huduma kwa mama wajawazito? Je unafikiri washirikiane vipi na wizara husika?

*Dr Riziki Ponsiano: HPV-vaccine project coordinator(MD, PGD-Mch, MPH-Social & Behvrl science) and Dr Tausi Kida ( PhD Dev Economics) ; Project Coordinator; ESRF/REPOA/ISS Capacity Building - Poverty Analysis

SHARE THIS

Author:

Previous Post
Next Post